News and Stories

Profesa John Gongwe Kiango, Jabali la Lugha za Kiafrika Duniani  05.09.1949 – 04.02.2026

Taasisi ya Lugha za Kiafrika (ACALAN) ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) imepoteza mmoja wa waanzilishi wake, Profesa John Gongwe Kiango, aliyefariki tarehe 4 Februari 2026 Jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania. 

Profesa Kiango ameifanyia ACALAN kazi kubwa sana akihudumu kama mtaalam wa lugha na Mratibu wa Kamisheni ya Kiswahili. Tunamtambua kama mtaalamu aliyetumia muda wake wote kuzipa nguvu lugha za Kiafrika. Ikumbukwe kwamba Profesa Kiango ndiye aliyeandika nyaraka ya awali (concept note) ya ACALAN kuhusu lugha za mipakani (cross border languages). Kazi iliyojenga msingi wa uanzishwaji wa kamisheni nyingine za lugha za mipakani barani Afrika.

Profesa Kiango alikuwa zaidi ya mwalimu, alikuwa mwongozo na msukumo kwenye lugha za Kiafrika duniani kote alipokwenda kuhudumu na kufanya mawasilisho. Kina cha usomi wake kililingana na unyenyekevu wake. Tunasikitika sana kwamba Profesa Kiango ameondoka wakati ACALAN inasherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, Jijini Bamako, Mali.

Ingawa tunaomboleza kumpoteza msomi jabali na mahiri, tunasherehekea maisha aliyojitolea kwa ajili ya kutafuta ukweli na uelewaji kwenye lugha za Kiafrika hasa Kiswahili. Akili kubwa imetuacha na imeacha nyuma urithi mkubwa wa taaluma ya lugha ambao utaendelea kutuongoza kwa miaka mingi ijayo.

Ni katika kutambua mchango wake katika makuzi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika, ACALAN inatoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wote wa Kiswahili na lugha za Kiafrika duniani.

Ingawa nuru angavu ya Profesa Kiango imezimika, kazi za kitaaluma na mafundisho ya yake yataendelea kuwa hai na kuendelea kutuangazia.

Tunamtakia Profesa Kiango safari njema na pumziko la amani tukiamini kwamba, msingi aliouweka ACALAN utabaki kuwa mwongozo kwa vizazi na vizazi. 

Wasalaam

Taasisi ya Lugha za Kiafrika (ACALAN)